Saturday, September 3, 2016

NGUZO ZA UTAWALA BORA 2

NGUZO ZA UTAWALA BORA 2

Dhana ya Utawala Bora ina nguzo kuu sita:
• Katiba ya kidemokrasia;
• Ulinzi, ukuzaji na uzingatiaji wa haki za binadamu;
• Mgawanyo wa Madaraka;
• Uhuru wa Mahakama;
• Uhuru wa habari na
• Uhuru wa vyombo vya habari.


MISINGI YA UTAWALA BORA

1 Uwazi
Uwazi ni hali ya kuendesha shughuli za umma bila usiri na kificho ili wananchi wawe na uwezo wa kupima utendaji na uzingatiaji wa kanuni, taratibu na sheria. Uwazi unajumuisha:

• Wananchi kupata taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti za kutekeleza mipango hiyo, kwa lugha rahisi na kwa wakati;
• Wananchi kupewa taarifa za mapato na matumizi;
• Wananchi kufahamishwa huduma zinazotolewa bila malipo na huduma wanazopaswa kuchangia, na utaratibu wa kupata huduma hizo;
• Wananchi kujulishwa mahali na wakati muafaka wa kupata taarifa wanazozihitaji na wazipate bila usumbufu; na
• Kupewa sababu na uhalali wa maamuzi yaliyofikiwa na viongozi wao.

2 Uwajibikaji

Uwajibikaji ni hali ya kiongozi na mtendaji kuwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo aliyoyafanya katika kutekeleza dhamana
aliyopewa. Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Serikali (viongozi na watendaji) itawajibika kwa wananchi.

Utawala wa Sheria

Utawala wa Sheria unamaanisha mambo yafuatayo:
• Mfumo wa sheria za nchi ulio wa haki na ambao umejengwa na sheria zisizo kandamizi;
• Usawa mbele ya sheria: watu wote wawe sawa mbele ya sheria;
• Uendeshaji wa shughuli za umma pamoja na maamuzi lazima vifanyike kwa kufuata sheria za nchi; na
• Ulinzi na haki sawa mbele ya sheria.

4 Ushirikishwaji

Ni kuwahusisha wananchi wa jinsia zote na makundi yote katika kupanga na kufanya maamuzi ya mambo yanayowahusu.
Ushirikishwaji unaweza ukawa wa moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi.

5 Usawa
Ni hali ya kuwapatia wananchi wote fursa sawa katika kushiriki kwenye mambo yanayohusu jamii yao. Usawa katika utendaji unahusisha mambo yafuatayo:
• Kutoa huduma bila ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote.
• Kuendesha shughuli za umma bila ubaguzi au upendeleo.
• Kuthamini watu wote bila kujali tofauti zao.
• Kutambua makundi yote katika jamii na kutoa fursa sawa kwa makundi yote katika kuboresha hali zao.
• Kumfanya kila mwanajamii kujiona kuwa yeye ni sehemu ya jamii na pia ana maslahi kwenye jamii yake.

6 Ufanisi na Tija.
Ufanisi na tija ni hali ya utendaji inayozalisha matokeo yanayokidhi malengo na matarajio ya watu na kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali. Ufanisi na Tija unajumuisha mambo yafuatayo:
• Utendaji wenye matokeo yanayokidhi malengo na matarajio ya watu wote.
• Kutumia rasilimali kwa uangalifu na umakini (Matumizi bora ya rasilimali).
• Utumiaji endelevu wa rasilimali.
• Utunzaji wa mazingira.
• Utoaji wa uhakika wa huduma za jamii.

7 Mwitikio
Ni hali ya kutoa huduma kwa jamii kwa wakati na kwa kiwango kinachokidhi matarajio ya watu. Mwitikio unajumuisha mambo yafuatayo:
• Kujali na kusikiliza matatizo ya watu.
• Kutoa huduma kwa haraka na kwa kiwango bora.
• Kukidhi matarajio ya watu.

8 Maridhiano
Utawala bora unahimiza kukutanishwa kwa mawazo mbalimbali ili kupata suluhu au maamuzi ya pamoja ambayo yanazingatia matakwa ya jamii nzima.

9 Uadilifu
Ni hali ya kuwa mwaminifu na kuwa na mwenendo mzuri katika utendaji kazi. Uadilifu unahusisha kujali watu, kujali muda, kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, kuepuka vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, kuwa mkweli, kufanya kazi kwa bidii na maarifa

No comments:

Post a Comment