Saturday, September 3, 2016

MJUE DIWANI

                                                      1. DIWANI NI NANI?


(i) Ni Mwakilishi wa wananchi kwenye Kata.
(ii) Ni Mjumbe wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri ya Mji,
Wilaya, Manispaa au Jiji).
(iii) Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata

2. KUNA AINA NGAPI ZA MADIWANI?

Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, zinataja aina nne za madiwani, ambao ni:
• Madiwani wa kuchaguliwa;
• Madiwani wa kuteuliwa;
• Madiwani wa viti maalum (wanawake); na
• Wabunge (wa kuchaguliwa au kuteuliwa).


3. DIWANI ANAPATIKANAJE?

(i) Kwa kuchaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano;
(ii) Kwa kuchaguliwa kwenye uchaguzi mdogo pindi nafasi ya Diwani inapokuwa wazi kwa sababu za: kifo cha Diwani; Diwani kukosa sifa za kuwa Diwani kwa mujibu wa sheria; kubatilishwa kwa uchaguzi wa Diwani; nafasi ya Diwani kuwa wazi kwa mujibu wa Sheria; na Diwani kukoma kuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichomteua akiwakilishe; na
(iii) Kwa kuteuliwa na chama chake (kwa madiwani wa kuteuliwa wa viti maalum).

4. SIFA ZA KUGOMBEA UDIWANI

Mtu anaweza kugombea na kuchaguliwa kuwa Diwani iwapo anakidhi
sifa zifuatazo:
(i) Awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(ii) Awe ametimiza umri wa miaka ishirini na moja au zaidi;
(iii) Awe na akili timamu;
(iv) Awe ni mkazi wa kawaida wa eneo la Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika;
(v) Anaweza kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza;
(vi) Awe ni mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 na chama chake kimemteua akiwakilishe kwenye uchaguzi husika;
(vii) Awe na njia halali za kujipatia kipato;
(viii) Asiwe amehukumiwa kwa kosa la ukwepaji kodi ndani ya kipindi cha miaka mitano kabla ya uchaguzi.
(ix) Asiwe amehukumiwa kifo au amehukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita jela.

5. DIWANI ANA MAJUKUMU GANI?

Majukumu ya Diwani yanatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287; Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288; na

Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Kwa ujumla Majukumu ya Diwani ni:

• Uwakilishi wa wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo
• Kuongoza wananchi kwa makini na uadilifu
• Usimamizi wa rasilimali na sheria
• Mgawaji wa Rasilimali kwa kufuata taratibu zilizowekwa
• Kusimamia Michakato ya Utungaji na upitishaji wa Sheria ndogo ndogo katika eneo lake la kazi
• Kuwawezesha wanajamiiwa eneo lake kupata fursa mbalimbali za kimaendeleo
• Kuongoza na kufanikisha wananchi wake katika kutatua migogoro mbalimbali katika kata
• Kuhamasisha shughuli za maendeleo katika eneo lake la kazi

6. DIWANI ANAWAWAKILISHA NANI?

Kifungu cha 14 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kinaeleza kuwa Diwani ni mwakilishi wa wananchi kwenye Kata aliyochaguliwa.

a.) Diwani kama Mwakilishi wa wananchi ana wajibu gani?

Diwani kama Mwakilishi wa wananchi ana wajibu ufuatao:

• Kuwakilisha wananchi wa Kata yake katika vikao vya Halmashauri.
• Kuhudhuria na kushiriki vikao vya Halmashauri.
• Kuwa kiungo kati ya wananchi na Halmashauri husika.
• Kutetea maslahi ya watu wa eneo analoliwakilisha.
• Kukutana na wananchi katika eneo lake ili kusikiliza na kuchukua maoni, mapendekezo, kero na matatizo ya watu wa eneo analoliwakilisha.
• Kutoa taarifa kwa wapiga kura kuhusu maamuzi ya jumla ya halmashauri na hatua zilizochukuliwa na Halmashauri ili kuondoa matatizo yaliyowahi kuelezwa na wakazi wa eneo lake la uchaguzi.
• Kusimamia na kudhibiti utumiaji wa rasilimali ya umma kupitia kamati za kudumu za madiwani.

b.) Je! Diwani ni Mwajiriwa wa Halmashauri?

Diwani si mwajiriwa wa Halmashauri, bali ni “Mwakilishi wa watu”, na hivyo anawajibika kwa watu anaowawakilisha na wakazi wa eneo la Halmashauri yake.

No comments:

Post a Comment