Saturday, September 3, 2016

MJUE DIWANI 2


7. DIWANI KAMA KIONGOZI ANA WAJIBU GANI?

• Kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.
• Kushirikisha wananchi katika uandaaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
• Kuitisha na kuendesha vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata (Ward Development Committee -WDC).
• Kushiriki katika kufikia maamuzi na kutoa maelekezo kupitia vikao halali vya baraza la madiwani.
• Kuhamasisha wananchi kutunza mazingira na kuhifadhi maliasili za nchi.
• Kushiriki katika kufikia maamuzi na kutoa maelekezo kupitia vikao halali vya baraza la madiwani.
• Kuhakikisha kwamba watumishi wote waliopo katika eneo la kata yake wanafanya kazi zao kwa uadilifu na ufanisi na endapo utendaji wao hauridhishi anapaswa kutoa taarifa kwenye kamati husika au kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri yake.
• Kuhamasisha utawala bora.
• Kuhamasisha wananchi kulipa kodi na ushuru wa Halmashauri husika.

a). Je! Diwani ni Mtendaji?

Diwani si Mtendaji, bali ni Kiongozi na Mwakilishi wa wananchi, hivyo:
• Diwani hapaswi kuingilia utendaji wa idara yoyote katika Halmashauri kwa maslahi yake binafsi.
• Diwani hapaswi kutoa maelekezo, amri au maagizo kwa mwajiriwa au wakala yoyote wa Halmashauri.
• Diwani hapaswi kuzuia au kujaribu kuzuia utekelezaji wa maamuzi ya baraza la madiwani au kamati au mwajiriwa au wakala wa Halmashauri.

8. DIWANI KAMA MSIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UMMA ANA WAJIBU GANI?

• Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya Baraza la Madiwani.
• Kufuatilia matumizi ya fedha za Halmashauri kwa lengo la kujiridhisha kuwa matumizi ya fedha hizo hayavuki bajeti iliyoidhinishwa na kwamba fedha zote zimetumika kwa madhumuni yaliyopangwa.
• Kusimamia matumizi bora ya rasilimali za umma kwenye Halmashauri yake.
• Kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata yake.
• Kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Taratibu, Kanuni, Miongozo, Sheria ndogo ndogo na miongozo ya Halmashauri.
• Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi, mipango na utoaji wa huduma katika kata yake na kutoa taarifa kwenye vikao vya Halmashauri au kamati za Halmashauri endapo kuna kasoro za msingi za utekelezaji.
• Kushiriki katika kufanya maazimio na maamuzi ya kuwawajibisha watendaji wazembe na wasio waadilifu.
• Kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

9. DIWANI KAMA MSIMAMIZI WA UGAWAJI WA RASILIMALI ANA WAJIBU GANI?

• Kuwashirikisha wananchi katika kuainisha vyanzo vya mapato, mahitaji, fursa na vipaumbele vyao.
• Kuhakikisha ukusanyaji na matumizi sahihi ya mapato kulingana na mahitaji na vipaumbele vya wananchi.
• Kusimamia mchakato mzima wa mipango na bajeti.
• Kuidhinisha makisio ya mapato na matumizi ya Halmashauri baada ya kuzingatia tathmini ya mahitaji na rasilimali zilizopo.
• Kuhakikisha kuwa kazi zilizopangwa zimetengewa bajeti.

10. KAMA JUKUMU LA KUTUNGA SHERIA NI LA BUNGE, DIWANI AMEPATA WAPI MAMLAKA YA KUTUNGA SHERIA?

Diwani amepewa mamlaka ya kusimamia na kutunga sheria ndogo ndogo na kifungu cha 153 (1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura 287, kifungu cha 89 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Mji), Sura 288 na Kifungu cha 122 (1) (d) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287. Mamlaka haya hutekelezwa kupitia vikao halali vya Baraza la Madiwani.

Uwezo huu wa kutunga Sheria ndogo ndogo unahusisha mambo mawili:

i) Kutunga Sheria ndogo zitakazotumika katika eneo la mamlaka yao; na
ii) kupitisha sheria ndogo ndogo zilizotungwa na Halmashauri za vijiji zilizopo katika eneo la mamlaka yao.

Sheria ndogo ndogo ni Zipi?

Sheria ndogo ndogo (by-laws) ni kanuni zilizotungwa kwa mujibu wa sheria ya bunge kwa ajili ya kurahisisha au kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya mamlaka husika au kusaidia utekelezaji wa sheria mama.

11. DIWANI KAMA MUWEZESHAJI ANA WAJIBU GANI?

i) Kusikiliza matatizo ya wananchi, kujadiliana na kuwashauri hatua za kuchukua mfano kutafuta mtaalam wa kilimo katika eneo lake
ii) Kuwezesha watu kupata taarifa muhimu kuhusu masuala ya maendeleo.
iii) Kuwasaidia wananchi waone fursa zinazowazunguka katika nyanja za sekta kuu kama uchumi, maji, afya, miundombinu, elimu na siasa.
iv) Kupitia wataalamu waliomo kwenye Kata yake, kuwawezesha wananchi kupata mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii kama vile kilimo, ujasiriamali, afya bora, makazi bora, n.k.
v) Kuhamasisha wananchi kujitegemea
vi) Kuondoa vikwazo vya kisheria na kiutawala, kama vile urasimu usio wa lazima.
vii) Kufanikisha ushirikishwaji wa wananchi katika mipango, utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo katika
maeneo yao.
viii) Kuhamasisha ulinzi wa amani, usalama, demokrasia, utawala bora na uzingatiaji wa sheria katika maeneo yao.

12. DIWANI ANATAKIWA KUWA NA MWENENDO GANI?

Diwani anapaswa kuwa na mwenendo wenye maadili mema kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Maadili na Mwenendo wa Madiwani (Tangazo la Serikali Na. 280 la mwaka 2000).

Kwa kifupi , Diwani anapaswa awe na mwenendo ufuatao:

• Kuendesha shughuli zake kwa kujenga imani ya wananchi
• Kuheshimu na kuzingatia sheria
• Kutotumia nafasi yake kwa faida yake, au familia yake, marafiki zake n.k.
• Kutojiweka katika hali ya mgongano na maslahi yake.
• Kuwajibika kwa jamii na Halmashauri yake kutokana na matendo yake na maamuzi ya Halmashauri.
• Kuwa muwazi, mkweli na muaminifu.
• Kufanya maamuzi bila upendeleo au ubaguzi na kwa kuzingatia sheria na haki.
• Kuhakikisha kuwa habari zote za siri za wananchi zinahifadhiwa kwa mujibu wa sheria, na hazitumiki kwa maslahi au faida binafsi.
• Kutoshiriki katika majadiliano au kupiga kura kuhusu jambo ambalo ana maslahi nalo.
• Kutoa taarifa kuhusu maslahi na mali zake pale inapobidi kufanya hivyo.
• Kuheshimu nafasi na hadhi ya madiwani wenzake na watumishi wa Halmashauri.
• Kutokuwa na uhusiano wa kimapenzi usiokubalika kati yake na Diwani mwenzake au watumishi wa Halmashauri.
• Kutoomba wala kupokea rushwa/hongo au zawadi kutoka kwa mtu anayemhudumia.
• Kutoingilia utendaji wa kazi wa idara yoyote katika halmashauri.

No comments:

Post a Comment