Saturday, September 3, 2016

MJUE DIWANI 2


7. DIWANI KAMA KIONGOZI ANA WAJIBU GANI?

• Kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.
• Kushirikisha wananchi katika uandaaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
• Kuitisha na kuendesha vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata (Ward Development Committee -WDC).
• Kushiriki katika kufikia maamuzi na kutoa maelekezo kupitia vikao halali vya baraza la madiwani.
• Kuhamasisha wananchi kutunza mazingira na kuhifadhi maliasili za nchi.
• Kushiriki katika kufikia maamuzi na kutoa maelekezo kupitia vikao halali vya baraza la madiwani.
• Kuhakikisha kwamba watumishi wote waliopo katika eneo la kata yake wanafanya kazi zao kwa uadilifu na ufanisi na endapo utendaji wao hauridhishi anapaswa kutoa taarifa kwenye kamati husika au kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri yake.
• Kuhamasisha utawala bora.
• Kuhamasisha wananchi kulipa kodi na ushuru wa Halmashauri husika.

a). Je! Diwani ni Mtendaji?

Diwani si Mtendaji, bali ni Kiongozi na Mwakilishi wa wananchi, hivyo:
• Diwani hapaswi kuingilia utendaji wa idara yoyote katika Halmashauri kwa maslahi yake binafsi.
• Diwani hapaswi kutoa maelekezo, amri au maagizo kwa mwajiriwa au wakala yoyote wa Halmashauri.
• Diwani hapaswi kuzuia au kujaribu kuzuia utekelezaji wa maamuzi ya baraza la madiwani au kamati au mwajiriwa au wakala wa Halmashauri.

8. DIWANI KAMA MSIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UMMA ANA WAJIBU GANI?

• Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya Baraza la Madiwani.
• Kufuatilia matumizi ya fedha za Halmashauri kwa lengo la kujiridhisha kuwa matumizi ya fedha hizo hayavuki bajeti iliyoidhinishwa na kwamba fedha zote zimetumika kwa madhumuni yaliyopangwa.
• Kusimamia matumizi bora ya rasilimali za umma kwenye Halmashauri yake.
• Kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata yake.
• Kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Taratibu, Kanuni, Miongozo, Sheria ndogo ndogo na miongozo ya Halmashauri.
• Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi, mipango na utoaji wa huduma katika kata yake na kutoa taarifa kwenye vikao vya Halmashauri au kamati za Halmashauri endapo kuna kasoro za msingi za utekelezaji.
• Kushiriki katika kufanya maazimio na maamuzi ya kuwawajibisha watendaji wazembe na wasio waadilifu.
• Kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

9. DIWANI KAMA MSIMAMIZI WA UGAWAJI WA RASILIMALI ANA WAJIBU GANI?

• Kuwashirikisha wananchi katika kuainisha vyanzo vya mapato, mahitaji, fursa na vipaumbele vyao.
• Kuhakikisha ukusanyaji na matumizi sahihi ya mapato kulingana na mahitaji na vipaumbele vya wananchi.
• Kusimamia mchakato mzima wa mipango na bajeti.
• Kuidhinisha makisio ya mapato na matumizi ya Halmashauri baada ya kuzingatia tathmini ya mahitaji na rasilimali zilizopo.
• Kuhakikisha kuwa kazi zilizopangwa zimetengewa bajeti.

10. KAMA JUKUMU LA KUTUNGA SHERIA NI LA BUNGE, DIWANI AMEPATA WAPI MAMLAKA YA KUTUNGA SHERIA?

Diwani amepewa mamlaka ya kusimamia na kutunga sheria ndogo ndogo na kifungu cha 153 (1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura 287, kifungu cha 89 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Mji), Sura 288 na Kifungu cha 122 (1) (d) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287. Mamlaka haya hutekelezwa kupitia vikao halali vya Baraza la Madiwani.

Uwezo huu wa kutunga Sheria ndogo ndogo unahusisha mambo mawili:

i) Kutunga Sheria ndogo zitakazotumika katika eneo la mamlaka yao; na
ii) kupitisha sheria ndogo ndogo zilizotungwa na Halmashauri za vijiji zilizopo katika eneo la mamlaka yao.

Sheria ndogo ndogo ni Zipi?

Sheria ndogo ndogo (by-laws) ni kanuni zilizotungwa kwa mujibu wa sheria ya bunge kwa ajili ya kurahisisha au kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya mamlaka husika au kusaidia utekelezaji wa sheria mama.

11. DIWANI KAMA MUWEZESHAJI ANA WAJIBU GANI?

i) Kusikiliza matatizo ya wananchi, kujadiliana na kuwashauri hatua za kuchukua mfano kutafuta mtaalam wa kilimo katika eneo lake
ii) Kuwezesha watu kupata taarifa muhimu kuhusu masuala ya maendeleo.
iii) Kuwasaidia wananchi waone fursa zinazowazunguka katika nyanja za sekta kuu kama uchumi, maji, afya, miundombinu, elimu na siasa.
iv) Kupitia wataalamu waliomo kwenye Kata yake, kuwawezesha wananchi kupata mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii kama vile kilimo, ujasiriamali, afya bora, makazi bora, n.k.
v) Kuhamasisha wananchi kujitegemea
vi) Kuondoa vikwazo vya kisheria na kiutawala, kama vile urasimu usio wa lazima.
vii) Kufanikisha ushirikishwaji wa wananchi katika mipango, utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo katika
maeneo yao.
viii) Kuhamasisha ulinzi wa amani, usalama, demokrasia, utawala bora na uzingatiaji wa sheria katika maeneo yao.

12. DIWANI ANATAKIWA KUWA NA MWENENDO GANI?

Diwani anapaswa kuwa na mwenendo wenye maadili mema kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Maadili na Mwenendo wa Madiwani (Tangazo la Serikali Na. 280 la mwaka 2000).

Kwa kifupi , Diwani anapaswa awe na mwenendo ufuatao:

• Kuendesha shughuli zake kwa kujenga imani ya wananchi
• Kuheshimu na kuzingatia sheria
• Kutotumia nafasi yake kwa faida yake, au familia yake, marafiki zake n.k.
• Kutojiweka katika hali ya mgongano na maslahi yake.
• Kuwajibika kwa jamii na Halmashauri yake kutokana na matendo yake na maamuzi ya Halmashauri.
• Kuwa muwazi, mkweli na muaminifu.
• Kufanya maamuzi bila upendeleo au ubaguzi na kwa kuzingatia sheria na haki.
• Kuhakikisha kuwa habari zote za siri za wananchi zinahifadhiwa kwa mujibu wa sheria, na hazitumiki kwa maslahi au faida binafsi.
• Kutoshiriki katika majadiliano au kupiga kura kuhusu jambo ambalo ana maslahi nalo.
• Kutoa taarifa kuhusu maslahi na mali zake pale inapobidi kufanya hivyo.
• Kuheshimu nafasi na hadhi ya madiwani wenzake na watumishi wa Halmashauri.
• Kutokuwa na uhusiano wa kimapenzi usiokubalika kati yake na Diwani mwenzake au watumishi wa Halmashauri.
• Kutoomba wala kupokea rushwa/hongo au zawadi kutoka kwa mtu anayemhudumia.
• Kutoingilia utendaji wa kazi wa idara yoyote katika halmashauri.

MJUE DIWANI

                                                      1. DIWANI NI NANI?


(i) Ni Mwakilishi wa wananchi kwenye Kata.
(ii) Ni Mjumbe wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri ya Mji,
Wilaya, Manispaa au Jiji).
(iii) Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata

2. KUNA AINA NGAPI ZA MADIWANI?

Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, zinataja aina nne za madiwani, ambao ni:
• Madiwani wa kuchaguliwa;
• Madiwani wa kuteuliwa;
• Madiwani wa viti maalum (wanawake); na
• Wabunge (wa kuchaguliwa au kuteuliwa).


3. DIWANI ANAPATIKANAJE?

(i) Kwa kuchaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano;
(ii) Kwa kuchaguliwa kwenye uchaguzi mdogo pindi nafasi ya Diwani inapokuwa wazi kwa sababu za: kifo cha Diwani; Diwani kukosa sifa za kuwa Diwani kwa mujibu wa sheria; kubatilishwa kwa uchaguzi wa Diwani; nafasi ya Diwani kuwa wazi kwa mujibu wa Sheria; na Diwani kukoma kuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichomteua akiwakilishe; na
(iii) Kwa kuteuliwa na chama chake (kwa madiwani wa kuteuliwa wa viti maalum).

4. SIFA ZA KUGOMBEA UDIWANI

Mtu anaweza kugombea na kuchaguliwa kuwa Diwani iwapo anakidhi
sifa zifuatazo:
(i) Awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(ii) Awe ametimiza umri wa miaka ishirini na moja au zaidi;
(iii) Awe na akili timamu;
(iv) Awe ni mkazi wa kawaida wa eneo la Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika;
(v) Anaweza kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza;
(vi) Awe ni mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 na chama chake kimemteua akiwakilishe kwenye uchaguzi husika;
(vii) Awe na njia halali za kujipatia kipato;
(viii) Asiwe amehukumiwa kwa kosa la ukwepaji kodi ndani ya kipindi cha miaka mitano kabla ya uchaguzi.
(ix) Asiwe amehukumiwa kifo au amehukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita jela.

5. DIWANI ANA MAJUKUMU GANI?

Majukumu ya Diwani yanatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287; Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288; na

Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Kwa ujumla Majukumu ya Diwani ni:

• Uwakilishi wa wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo
• Kuongoza wananchi kwa makini na uadilifu
• Usimamizi wa rasilimali na sheria
• Mgawaji wa Rasilimali kwa kufuata taratibu zilizowekwa
• Kusimamia Michakato ya Utungaji na upitishaji wa Sheria ndogo ndogo katika eneo lake la kazi
• Kuwawezesha wanajamiiwa eneo lake kupata fursa mbalimbali za kimaendeleo
• Kuongoza na kufanikisha wananchi wake katika kutatua migogoro mbalimbali katika kata
• Kuhamasisha shughuli za maendeleo katika eneo lake la kazi

6. DIWANI ANAWAWAKILISHA NANI?

Kifungu cha 14 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kinaeleza kuwa Diwani ni mwakilishi wa wananchi kwenye Kata aliyochaguliwa.

a.) Diwani kama Mwakilishi wa wananchi ana wajibu gani?

Diwani kama Mwakilishi wa wananchi ana wajibu ufuatao:

• Kuwakilisha wananchi wa Kata yake katika vikao vya Halmashauri.
• Kuhudhuria na kushiriki vikao vya Halmashauri.
• Kuwa kiungo kati ya wananchi na Halmashauri husika.
• Kutetea maslahi ya watu wa eneo analoliwakilisha.
• Kukutana na wananchi katika eneo lake ili kusikiliza na kuchukua maoni, mapendekezo, kero na matatizo ya watu wa eneo analoliwakilisha.
• Kutoa taarifa kwa wapiga kura kuhusu maamuzi ya jumla ya halmashauri na hatua zilizochukuliwa na Halmashauri ili kuondoa matatizo yaliyowahi kuelezwa na wakazi wa eneo lake la uchaguzi.
• Kusimamia na kudhibiti utumiaji wa rasilimali ya umma kupitia kamati za kudumu za madiwani.

b.) Je! Diwani ni Mwajiriwa wa Halmashauri?

Diwani si mwajiriwa wa Halmashauri, bali ni “Mwakilishi wa watu”, na hivyo anawajibika kwa watu anaowawakilisha na wakazi wa eneo la Halmashauri yake.

ELimu Y Uraia kupelekwa Bungeni.

                                                   ELimu Y Uraia kupelekwa Bungeni
.

Makamu wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN ameiomba Taasisi ya HANNS SEIDEL FOUNDATION isaidie kupeleka elimu ya uraia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa TANZANIA ili Wabunge wa bunge hilo waweze kujua wajibu wao ndani na nje ya bunge.
SAMIA ametoa ombi hilo Ikulu Jijini DSM alipokutana na ujumbe wa Taasisi hiyo uliomtembelea ofisi kwake kwa lengo la kutaka kujua kama ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa TANZANIA kuna sheria na kanuni za kuendesha vikao vya Bunge.

Makamu wa Rais Ameueleza ujumbe huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Hanns Seidel Foundation Profesa URSULA MANNK kuwa sheria na kanuni zipo za kuendesha vikao vya Bunge lakini baadhi ya wabunge hawazifuati kama inavyotakiwa.

Tasisi ya Hanns Seidel Foundation yenye makao yake makuu yake Mjini MUNICH nchini UJERUMANI inajishughulisha na masuala ya demokrasia, amani na maendeleo na inaendesha shughuli zake katika nchi zaidi ya 60 duniani.
August 11, 2016
TBC-Taarifa

NINI MAANA YA UONGOZI?

NINI MAANA YA UONGOZI?

 Uongozi ni mamlaka au karama ya kuonyesha njia kwa vitendo.
Kipimo cha uongozi ni jinsi gani kiongozi anaweza kuleta ushawishi kwa watu na kufikia maendeleoyaliyotarajiwa. Kiongozi bora hana muda wa kulalamika bali anatafuta ufumbuzi wa matatizo ya watu, yaani wananchi au watu walio chini yake. Kiongozi wa kweli akiongea, watu husikiliza.
Maana ya uongozi

Uongozi ni dhana, taaluma inayompa mhusika madaraka na uwezo wa kuwawezesha wale wanaongozwa naye kuunganisha nguvu, stadi na vipaji vyao na kuvitumia ili kufikia malengo yao. Kuongoza ni kujua lengo la wale wanaoongozwa na njia ya kufikia lengo lao.
Uongozi ni dhana, taaluma anayopewa mhusika katika kuwaongoza wale waliohitaji kusimamiwa au walioamuliwa kusimamiwa katika kufanikisha jambo fulani kwa maslahi ya wote au ya mtu mmoja mmoja.

Aina za uongozi

i) Kuna njia nyingi za kuainisha uongozi lakini njia ya msingi ni kuangalia jinsi kiongozi alivyoingia madarakani na utaratibu wake wa kuongoza.
ii) Katika viongozi wapo Wafalme, Marais, Mawaziri, Watemi, Machifu, Wakurugenzi n.k.
iii) Viongozi hawa wote tunaweza kuwagawa katika mafungu yafuatayo kutokana na jinsi walivyoingia madarakani na namna wanavyoongoza kama ifuatavyo: i. Wale wanaopata uongozi kwa kurithi. ii. Wanaopata uongozi kwa kuchaguliwa. iii. Wanaojitwalia mamlaka ya kuongoza kwa nguvu. iv. Wanaoteuliwa na mamlaka za juu zaidi.
iv) Kiongozi anayeingia madarakani kwa mojawapo ya njia zilizotajwa hapa juu anaweza kutumia mtindo wake wa uongozi. Ipo mitindo mbalimbali ya uongozi: i. Uongozi wa kimila ii. Uongozi wa kidemokrasia. iii. Uongozi wa kiimla ni mtindo wa kuongoza ambao kiongozi huongoza kwa amri bila kushirikisha watu wengine katika kufanya maamuzi. Mara nyingi uongozi wa aina hii haulengi katika kukidhi maslahi ya walio wengi, bali tu ya yule anayeongoza na wale wanaomlinda. iv. Uongozi wa kidemokrasia ni ule wa kushirikisha watu katika kufanya maamuzi na utekelezaji wake. Kwa kawaida viongozi wa aina hii hulenga kukidhi mahitaji ya walengwa.
NB:Viongozi wanaochaguliwa mara nyingi huwa wanapewa muda wa kuongoza,na wale viongozi wa wanaojiteua hujipatia wao wenyewe muda wa kuongoza au hata hapo watakapo amua kuachia madaraka.

Sifa za kiongozi bora

i. Awe na ufahamu. Kiongozi ni lazima awe na ufahamu mkubwa juu ya taasisi anayoiongoza, malengo yake, mazingira na matatizo yake.
ii. Awe mwaminifu. Kila taasisi inalenga kufikia shabaha fulani. Ni wajibu wa kiongozi kuwaongoza wanataasisi ili wafikie malengo yao. Kwa hiyo kiongozi ni lazima aweze kubuni mikakati na mbinu zitakazoiwezesha taasisi anayoongoza kufikia malengo yake.
iii. Mwenye Maadili mema. Kiongozi ni lazima akubalike katika jamii na taasisi anayoiongoza. Ili akubalike ana budi kuzingatia maadili ya msingi ya jamii na taasisi yake. Kiongozi mwongo, mlevi, mvivu, asiye mwaminifu n.k. hawezi kuwa kiongozi mzuri.
iv. Amche Mungu.
v. Mwenye kukubalika na watu anaowaongoza.
vi. Mwenye kuwaongoza watu katika misingi bora ya uongozi bila kujari jinsia,rangi,ubini wala ukabila.

NGUZO ZA UTAWALA BORA 2

NGUZO ZA UTAWALA BORA 2

Dhana ya Utawala Bora ina nguzo kuu sita:
• Katiba ya kidemokrasia;
• Ulinzi, ukuzaji na uzingatiaji wa haki za binadamu;
• Mgawanyo wa Madaraka;
• Uhuru wa Mahakama;
• Uhuru wa habari na
• Uhuru wa vyombo vya habari.


MISINGI YA UTAWALA BORA

1 Uwazi
Uwazi ni hali ya kuendesha shughuli za umma bila usiri na kificho ili wananchi wawe na uwezo wa kupima utendaji na uzingatiaji wa kanuni, taratibu na sheria. Uwazi unajumuisha:

• Wananchi kupata taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti za kutekeleza mipango hiyo, kwa lugha rahisi na kwa wakati;
• Wananchi kupewa taarifa za mapato na matumizi;
• Wananchi kufahamishwa huduma zinazotolewa bila malipo na huduma wanazopaswa kuchangia, na utaratibu wa kupata huduma hizo;
• Wananchi kujulishwa mahali na wakati muafaka wa kupata taarifa wanazozihitaji na wazipate bila usumbufu; na
• Kupewa sababu na uhalali wa maamuzi yaliyofikiwa na viongozi wao.

2 Uwajibikaji

Uwajibikaji ni hali ya kiongozi na mtendaji kuwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo aliyoyafanya katika kutekeleza dhamana
aliyopewa. Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Serikali (viongozi na watendaji) itawajibika kwa wananchi.

Utawala wa Sheria

Utawala wa Sheria unamaanisha mambo yafuatayo:
• Mfumo wa sheria za nchi ulio wa haki na ambao umejengwa na sheria zisizo kandamizi;
• Usawa mbele ya sheria: watu wote wawe sawa mbele ya sheria;
• Uendeshaji wa shughuli za umma pamoja na maamuzi lazima vifanyike kwa kufuata sheria za nchi; na
• Ulinzi na haki sawa mbele ya sheria.

4 Ushirikishwaji

Ni kuwahusisha wananchi wa jinsia zote na makundi yote katika kupanga na kufanya maamuzi ya mambo yanayowahusu.
Ushirikishwaji unaweza ukawa wa moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi.

5 Usawa
Ni hali ya kuwapatia wananchi wote fursa sawa katika kushiriki kwenye mambo yanayohusu jamii yao. Usawa katika utendaji unahusisha mambo yafuatayo:
• Kutoa huduma bila ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote.
• Kuendesha shughuli za umma bila ubaguzi au upendeleo.
• Kuthamini watu wote bila kujali tofauti zao.
• Kutambua makundi yote katika jamii na kutoa fursa sawa kwa makundi yote katika kuboresha hali zao.
• Kumfanya kila mwanajamii kujiona kuwa yeye ni sehemu ya jamii na pia ana maslahi kwenye jamii yake.

6 Ufanisi na Tija.
Ufanisi na tija ni hali ya utendaji inayozalisha matokeo yanayokidhi malengo na matarajio ya watu na kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali. Ufanisi na Tija unajumuisha mambo yafuatayo:
• Utendaji wenye matokeo yanayokidhi malengo na matarajio ya watu wote.
• Kutumia rasilimali kwa uangalifu na umakini (Matumizi bora ya rasilimali).
• Utumiaji endelevu wa rasilimali.
• Utunzaji wa mazingira.
• Utoaji wa uhakika wa huduma za jamii.

7 Mwitikio
Ni hali ya kutoa huduma kwa jamii kwa wakati na kwa kiwango kinachokidhi matarajio ya watu. Mwitikio unajumuisha mambo yafuatayo:
• Kujali na kusikiliza matatizo ya watu.
• Kutoa huduma kwa haraka na kwa kiwango bora.
• Kukidhi matarajio ya watu.

8 Maridhiano
Utawala bora unahimiza kukutanishwa kwa mawazo mbalimbali ili kupata suluhu au maamuzi ya pamoja ambayo yanazingatia matakwa ya jamii nzima.

9 Uadilifu
Ni hali ya kuwa mwaminifu na kuwa na mwenendo mzuri katika utendaji kazi. Uadilifu unahusisha kujali watu, kujali muda, kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, kuepuka vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, kuwa mkweli, kufanya kazi kwa bidii na maarifa

UTAWALA BORA 1

SEHEMU YA KWANZA

UTAWALA BORA

Utawala ni matumizi ya mamlaka ya kisiasa, kiuchumi au
vinginevyo katika kusimamia masuala ya nchi kwenye ngazi
zote.
Utawala bora ni matumizi ya mamlaka ambayo yanakuwa na
uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu
usawa na unafuata utawala wa sheria.

Ili kutekeleza dhana ya utawala bora mambo yafuatayo lazima
yazingatiwe:
• Matumizi sahihi ya dola,
• Matumizi mazuri ya rasilimali kwa faida ya wananchi,
• Matumizi mazuri ya madaraka yao,
• Kujua na kutambua madaraka waliyonayo na matumizi
yake,
• Madaraka yanatumika kulingana na mipaka iliyowekwa na
katiba na sheria.
Utawala ni matumizi ya mamlaka ya kisiasa, kiuchumi au
vinginevyo katika kusimamia masuala ya nchi kwenye ngazi
zote.
Utawala bora ni matumizi ya mamlaka ambayo yanakuwa na
uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu
usawa na unafuata utawala wa sheria.

Ili kutekeleza dhana ya utawala bora mambo yafuatayo lazima
yazingatiwe:
• Matumizi sahihi ya dola,
• Matumizi mazuri ya rasilimali kwa faida ya wananchi,
• Matumizi mazuri ya madaraka yao,
• Kujua na kutambua madaraka waliyonayo na matumizi
yake,
• Madaraka yanatumika kulingana na mipaka iliyowekwa na
katiba na sheria.

Faida za Utawala Bora

Utawala bora unasaidia kuwa na mambo yafuatayo:
• Matumizi mazuri ya rasilimali za nchi,
• Maendeleo endelevu,
• Kupungua kwa umasikini, ujinga na maradhi,
• Kutokomea kwa rushwa,
• Huduma bora za jamii,
• Amani na utulivu,
• Kuheshimiwa kwa haki za binadamu,
• Utatuzi wa migogoro kwa mujibu wa sheria na taratibu,
• Kuleta ustawi wa wananchi.

HAKI ZA BINADAMU

HAKI ZA BINADAMU

Haki za binadamu ni stahili alizonazo kila binadamu kwa asili
ya kuwa binadamu.
Vyanzo vya Haki za Binadamu nchini Tanzania
Chanzo kikuu cha haki za binadamu nchini Tanzania ni Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Sambamba
na Katiba, vipo vyanzo vingine vya haki za binadamu nchini,
kama vile, Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009, Sheria
ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010, Sheria ya
Kuzuia na Kudhibiti Ukimwi Namba 28 ya mwaka 2008, Sheria
ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004, Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 (R.E. 2002) na
mikataba mbalimbali ya haki za binadamu ya kimataifa na ya
kikanda ambayo Tanzania imeisaini na kuiridhia.